Waziri wa kilimo nchini Mithika Linturi, amewarai wakulima walio na mahindi katika maghala yao kuuza mahindi hayo, ili kuepuka hasara ya kupungua kwa bei, mara serikali itakapoanza uagizaji wa mahindi kutoka katika mataifa ya nje.

Akiwahutubia wenyeji wa eneo la Talek Narok magharibi baada ya kukagua jinsi zoezi la usambazaji wa mbolea ya ruzuku katika kaunti za Narok, Bomet na Nakuru inaendelea, Linturi pia ametoa wito kwa wakulima kote nchini kujisajili na serikali ili kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo kwa wakati na kwa bei nafuu.

Aidha ameahidi kwamba serikali haitafanya uagizaji wa chakula wakati kuna chakula cha kutosha, na badala yake itafanya uagizaji kama suluhu ya muda mfupi.

Kuhusiana na zoezi la usambazaji wa Mbolea, Waziri huyo alieleza kuridhishwa na jinsi shughuli yenyewe inatekelezwa, huku akituma onyo kwa watakaopatikana wakijihusisha na uuzaji wa mbolea hizo kwa kupakia katika mifuko tofauti. Pia amewataka wakulima kuendelea kujisajili ili kuiwezesha serikali kuwashughulikia ipasavyo.

March 18, 2023