Utafiti mpya umefichua utendakazi wa serikali ya Rais William Ruto katika miezi sita ya kwanza madarakani, kulingana na Wakenya.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya utafiti TIFA unaonyesha kuwa Wakenya wanajali zaidi kuhusu gharama ya juu ya maisha.

Asilimia 37 ya waliohojiwa walitaja ongezeko la hali ngumu ya kiuchumi kama suala kuu ambalo Rais Ruto ameshindwa kutatua hadi sasa.

Asilimia 14 ya waliohojiwa, walimlaumu mkuu wa nchi  kwa kutotimiza ahadi za kampeni, huku asilimia tisa wakitaja ongezeko la kiwango cha ufisadi pamoja na kufutwa kwa kesi kuu za ufisadi.

Hata hivyo walipoulizwa kuhusu mafanikio ya utawala wa Rais Ruto, asilimia 29 ya waliohojiwa walitoa mfano wa uzinduzi wa Hustler Fund, huku asilimia tano wakiwa na furaha kuhusu kupunguzwa kwa gharama ya mbolea.

Asilimia nne wakati huo huo walitaja kuimarishwa kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kuhusiana na vipaumbele, asilimia 71 ya wakenya wamependekeza kupunguzwa kwa gharama ya maisha kwa, asilimia 49 wameitaka serikali kubuni nafasi za kazi huku asilimia 22 wakipendekeza  kushughulikiwa kwa maswala katika mfumo wa elimu.

TIFA ilisema ilifanya utafiti huo kati ya Machi 11 na 19, na zaidi ya wahojiwa 2,065 walishiriki.

March 29, 2023