BY ISAYA BURUGU,7TH APRIL,2023-Taharuki ingali imetanda  katika Kijiji cha Lami nyeusi kaunti a pokot magharibi baada ya Watu watano kuawa jana na  majambazi waliokuwa na silaha kali walipovamia Kijiji hicho.Mtu mwingine anauguza majeraha ya risasi kufuatia shambulio hilo, polisi na wenyeji walisema.

Wenyeji walisema wavamizi hao wanaoshukiwa kuwa katika harakati za kulipiza kisasi walivamia kijiji hicho siku ya Jumatano usiku na kufanikiwa kuiba mbuzi 19.Washambuliaji hao wanasemekana kuwapiga risasi watu sita waliokuwa wamelala na kuua watano kati yao papo hapo.

Mtu wa sita, mwanamke, alijeruhiwa vibaya, polisi walisema.Mkazi mmoja alisema washambuliaji walishambulia mwendo wa saa nane usiku wakiwa na silaha nzito.Kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi Apollo Okelo alisema timu ya maafisa wa usalama imetumwa katika eneo jirani la Kainuk kuwasaka majambazi hao.

Alisema hakuna mtu aliyekamatwa hadi sasa.Ni shambulio la hivi punde katika eneo hilo ambalo liko chini ya operesheni inayoendelea ya usalama.Kaunti sita za North Rift zilitangazwa kuwa hatari na kutatizika kuwezesha shughuli hiyo kuendelea.

April 7, 2023