Timu ya usalama inayoendesha oparesheni katika maeneo yanayoshuhudia utovu wa usalama ilifanikiwa kurejesha mbuzi 25 na kondoo 16 waliokuwa wameibiwa na majambazi huko Baringo Kusini.

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPS, timu hiyo ilipokea simu kwamba majambazi wamevamia na kuiba mifugo katika eneo la Lamaiwe huko Baringo.

Kilichofuata ilikuwa ni majibizano makali ya risasi ambayo yalisababisha kupatikana kwa wanyama wote ambao wamekabidhiwa kwa mmiliki.


Siku tano zilizopita, ng’ombe 28 na mbuzi 24 walipatikana katika Bonde la Tandare katika operesheni sawia. Operesheni inayoendelea ya Maliza Uhalifu North Rift inalengwa katika kaunti sita zinazokabiliwa na majambazi.

Kaunti hizo ni pamoja na Laikipia, Baringo, Pokot Magharibi, Samburu, Elgeyo Marakwet na Turkana.

Operesheni hiyo inayoongozwa na polisi inasaidiwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya huku serikali ikiimarisha juhudi za kuwaondoa majambazi katika mikoa hiyo ambapo takriban watu 135 wakiwemo maafisa wa usalama 20 wameuawa katika muda wa miezi saba iliyopita.

April 10, 2023