BY ISAYA BURUGU,12TH APRIL,2023-Mwanamke mmoja anazuliwa katika kituo cha polisi  cha Muthaiga baada ya kuhusishwa na shehena haramu ya sigara iliyopatikana katika nyumba moja ya makazi, eneo la Kahawa West, Kaunti ya Nairobi.

Veronicah Njeri Kariuki anawasaidia wapelelezi katika uchunguzi wa sigara zinazokadiriwa kuwa za thamani ya shilingi milioni 30.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeripoti kwamba shehena hiyo iliyopatikana Jumanne inaaminika kuingizwa nchini kwa njia haramu.

“Shehena hiyo inayojumuisha zaidi ya pakiti 20,000 za chapa maarufu za sigara za Supermatch na Palma Safari ilinaswa na timu ya siri iliyojifanya wateja watarajiwa katika nyumba ya makazi karibu na barabara ya Riara, karibu na Shra Engineering huko Kahawa Magharibi, Kaunti ya Nairobi,” taarifa ya DCI ilisoma.

Wapelelezi walifichua kwamba mihuri bandia ya mamlaka ya ushuru ya Kenya (KRA) na ya Uganda (URA) iliweza kupatikana kwenye nyumba hiyo. Zilizopatikana pia ni masanduku tupu yaliyoandikwa British American Tobacco (BAT), Kenya na Supermatch.

April 12, 2023