Rais William Ruto ameunda Tume ya Uchunguzi inayojumuisha wanachama 13 kuanza uchunguzi kuhusu dhehebu la mhubiri Paul Mckenzie ambapo zaidi ya watu 100 wameripotiwa kufariki kufikia sasa.
Rais Ruto, katika notisi ya gazeti la serikali iliyotolewa Ijumaa, alitaja wanachama 8 wa tume hiyo itakayoongozwa na Jaji Jessie Lesiit.
Wajumbe wengine watakuwa; jaji Mary Muhanji Kasango, Eric Gumbo, Askofu Catherine Mutua, Dkt. Jonathan Lodompui, Dkt. Frank Njenga, Wanyama Musiambu na Albert Musasia.
Rais Ruto pia aliwateua Vivian Janet Nyambeki na Bahati Mwamuye kuwa mawakili wasaidizi wa tume hiyo. Mkuu wa nchi katika notisi hiyo, aliipa tume hiyo jukumu la kuchunguza vifo hivyo pamoja na madai ya kuteswa na kuwatendea kinyama wafuasi wa Mackenzie na kanisa lake la Good News International lenye makao yake makuu katika Kaunti ya Kilifi.
Timu hiyo pia itachunguza mazingira ambayo vifo hivyo vilitokea, na kuchunguza makosa ya kisheria, kitaasisi, kiutawala, kiusalama na ya kijasusi ambayo yanaweza kuwa yamechangia kutokea kwa mkasa wa Shakahola.
Aidha aliongeza kuwa tume hiyo inapaswa kupendekeza hatua za kisheria, kiutawala, au aina nyingine za uwajibikaji dhidi ya afisa yeyote wa umma ambaye hatua au kutotenda kwake kunathibitisha kuwa kumechangia kwa makusudi au kwa uzembe kutokea kwa Janga la Shakahola.