Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja,Raila Odinga, amepinga vikali mapendekezo ya Mswada wa Fedha wa 2023 uliowasilishwa Bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari Bw. Odinga amedokeza kuwa atafanya kila awezalo kuzuia Mswada huo kupitishwa katika Bunge la Kitaifa. Kiongozi huyo wa Azimio aliteta kuwa Wakenya wanatozwa ushuru kupita kiasi.
Kulingana na Raila, kuna ufisadi ulioandikwa kote katika Mswada huo ambao anasema kupandisha Ushuru wa Mauzo hadi 3% kutaathiri wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa kutoza ushuru wa mauzo yao ya jumla bila kujali kama wanapata faida au la.
Badala yake, kiongozi wa Azimio alipendekeza kwamba ushuru usalie kuwa 1%, inayotumika kwa mauzo ya jumla ya Ksh.1 milioni au zaidi.
Kando na hayo aliongeza kuwa mapendekezo ya marekebisho ya ushuru wa mapato yatazidisha mzigo kwa Wakenya, ambao wengi wao hawajapata nyongeza ya mishahara katika miaka mitano iliyopita.
Alidai kuwa ushuru wa moja kwa moja utapunguza mapato ya nchi na kuwa na athari kwa sekta zote za uchumi.
Wakati huo huo, alilenga hazina ya Nyumba iliyopendekezwa, akidai kwamba pendekezo la kukatwa kwa mishahara ya asilimia 3 ili kufadhili nyumba za bei nafuu ni “bila busara” ikizingatiwa kuwa wafanyikazi wengi tayari wanashughulika na mapato yaliyopunguzwa kwa sababu ya gharama ya juu ya maisha
.Pia alitilia shaka mantiki ya pendekezo la Mahakama ya Rufaa ya Ushuru ambayo itahitaji watu binafsi au wafanyabiashara kuweka 20% ya pesa zinazozozaniwa na KRA kabla ya kesi kusikizwa.