Maafisa wa polisi wanaowasaka manusura katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi sasa wataendeleza shughuli ya uokoaji hadi katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.

Waziri wa usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kithure Kindiki alisema Serikali itajumuisha msako wa ndege zisizo na rubani ili kuhakikisha manusura wote wanaokolewa.

Waziri huyo alibaini kuwa zoezi la pili la ufukuaji miil katika ardhi hiyo ya ekari 800 lilisitishwa ili kuruhusu serikali kufanya uchunguzi wa miili 123 iliyopatikana.

Uchunguzi wa miili hiyo utaanza Jumatano tarehe 24 Mei 2023 katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi. Hadi sasa idadi ya waliofariki imefikia 235 huku watu 613 wanaohusishwa na dhehebu la Paul Mckenzie wakiripotiwa kupotea.

May 20, 2023