Spika wa bunge la seneti Amason Kingi ameitisha kikao maalum cha seneti kuangazia ripoti ya kamati maalum iliyobuniwa kumchunguza Naibu Gavana wa Siaya William Oduol kufuatia kutimuliwa kwake na bunge la kaunti ya Siaya.

Katika notisi ya gazeti la serikali ya Juni 22, Kingi anawataka maseneta kuzingatia Ripoti ya Kamati hiyo maalum kuhusu Pendekezo la Kuondolewa afisini kwa Naibu Gavana huyo.Kikao hicho kitafanyika Jumatatu alasiri katika Bunge la Seneti kuanzia saa 8.30 asubuhi.

Oduol alibanduliwa ofisini baada ya wajumbe wote 42 wa bunge la kaunti ya siaya kupiga kura kwa kauli moja na kuidhinisha kuondolewa kwake kwa madai ya utovu wa nidhamu na utumizi mbaya wa afisi.

Katika madai yao, walitaja ununuzi wa kiti chenye thamani ya shilingi milioni 1.12 na miamala mingine kadhaa ya takriban shilingi milioni 18 ambazo walisema zilitumika kinyume cha sheria kwa ajili ya kumfariji Naibu Gavana.

Aidha akiwa mbele ya kamati maalum ya kumchunguza inayoongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet William Kisang`, Oduol alikanusha mashtaka yote dhidi yake.

June 23, 2023