Wanachama wa Jopo litakalo wapiga msasa wagombea wa wadhfa wa  mkurugenzi wa mashtaka ya umma uliokuwa ukishikiliwa na  Noordi Haji wamekula kiapo hii leo.

Wanachama hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli, Afisa mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak, na Wakili Mkuu Shadrack Mose.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Mary Kimonye, Mary Adhiambo Maumga, Roseline Odede, na Richard Onsongo Bush Obwocha.

Jopo hilo sasa litateua mwenyekiti ambaye ataongoza timu katika uhakiki wa walioteuliwa.

Akiongoza hafla ya kuapishwa kwa wanachama hao, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Anthony Muchiri aliitaka kamati hiyo kuzingatia uadilifu na haki katika mchakato wa uteuzi.

Haji aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa bosi mpya wa NIS mnamo Mei 16, 2023, kabla ya kuchunguzwa na kuidhinishwa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni mnamo Juni 13, 2023.

June 27, 2023