Hatimaye Familia tano zilizowapoteza wapendwa wao kwenye mashambulio ya kigaidi yaliyotekelezwa katika vijiji vya Salama na Juhudi mnamo Jumamosi usiku zimepokea msaada wa fedha za mazishi kwa wapendwa wao.

Kila familia imepokezwa Sh.100,000 na Gavana wa Lamu Issa Timamy kwa minajili ya kusimamia gharama ya mazishi.

Akizungumza kwenye shule ya Juhudi baada ya kutembelea vijiji vilivyoathirika, Bw.Timamy ameelezea kusikitishwa kwake na jinsi magaidi wanavyoendelea kutekeleza mashambulio ya kila mara katika kaunti hiyo ambapo watu huuwawa na mali kuharibiwa.

Magaidi waliojihami kwa silaha hatari ikiwemo bunduki, mapanga na visu walivamia vijiji vya Salama na Juhudi majira ya saa moja unusu jioni ya Jumamosi Juni 24,2023, ambapo waliwaua kwa kuwachinja wanaume, ikiwemo mwanafunzi wa miaka 19 wa shule ya upili ya Bakanja.

June 29, 2023