Saba saba

Mrengo wa upinzani nchini unapanga kuanza mchakato wa kukusanya saini milioni 10 ifikapo mwisho wa juma lijalo, lengo likiwa ni kuwezesha kuanzishwa kwa mchakato wa kumbandua mamlakani kiongozi wa Taifa, Rais William Ruto.

Hatua hii imechukuliwa baada ya kinara wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, kutangaza mpango huo katika uwanja wa Kamukunji, ambapo aliwaongoza wafuasi wake katika mkutano wa hadhara kabla ya kuanza kwa maandamano ya uasi kupinga utawala wa serikali ya Kenya Kwanza.

Leo, siku ya Saba Saba, maandamano yamekuwa taswira kuu nchini Kenya, ambapo maafisa wa polisi na waandamanaji wamekabiliana katika vita vya paka na panya katika miji mbalimbali. Jijini Nairobi, maafisa wa polisi wamekabiliwa na changamoto kubwa katika kuwadhibiti waandamanaji waliokuwa wakiongozwa na Raila Odinga, ambao walitaka kuvamia eneo la katikati mwa jiji. Maandamano hayo yalianzia katika uwanja wa Kamukunji na yalilenga kuelekea Uhuru Park, kabla ya viongozi hao kuelekea kwenye wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga ambapo tamko lingine lilitolewa. Odinga na viongozi wenzake walikosoa maafisa wa polisi kwa kuvuruga zoezi la kikatiba lililokuwa likiendeshwa kwa amani.

Vilevile, maandamano sawia yaliandaliwa katika maeneo mengine nchini. Kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, na mwenzake wa Narc Kenya, Martha Karua, wameongoza maandamano katika kaunti ya Machakos na Kirinyaga mtawalia. Kalonzo aliwaongoza viongozi wa upinzani na wananchi katika maandamano yaliyofanyika kwenye soko la Kathiani mjini Machakos, wakitoa wito kwa serikali kupunguza gharama ya maisha. Martha Karua, kwa upande wake, amezindua zoezi la ukusanyaji wa sahihi katika eneo la Difathas huko Kirinyaga, kuanzisha mchakato wa kumtimua rais mamlakani.

Mrengo wa upinzani una nia ya kuendeleza jitihada zake za kuhamasisha umma na kukusanya saini milioni 10 ili kuunga mkono mchakato wa kumbandua Rais William Ruto. Hatua hii hata hivyo huenda ikazua mjadala mkubwa nchini kuhusu mwelekeo wa kisiasa na mustakabali wa uongozi wa taifa.

July 7, 2023