Narok Muziki

Wafanyabiashara mjini Narok wameeleza furaha yao kutokana na faida kubwa katika biashara zao kwenye tamasha za muziki za shule za Msingi na Upili. Makala ya 95 ya tamasha za ukanda wa bonde la Ufa zinaendelea katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara mjini Narok.

Wafanyabiashara wamesifia athari chanya ambazo tamasha hizi zimeleta katika uchumi wa kaunti hii tangu zilipoanza Alhamisi iliyopita. Zaidi ya washiriki 1500 kutoka ukanda wa bonde la Ufa wanahudhuria mashindano ya mwaka huu, kuwatafuta mabingwa watakaopeperusha bendera ya kanda huu katika ngazi ya kitaifa.

Bw. Ibrahim Sankale ambaye ni mwenyekiti wa wapiga Picha mjini Narok amesema kwamba wamepokea idadi kubwa ya kazi za kuwapiga picha washiriki wa tamasha na matukio mbalimbali yanayojiri katika ukumbi wa mashindano. Hata hivyo Sankale amelalamikia malipo wanayotozwa ili kuruhusiwa kuendeleza biashara zao, jambo ambalo ametaka liangaziwe.

Wauzaji wa vyakula kwa upande wao nao wamerekodi ongezeko kubwa la mauzo kutokana na mahitaji ya chakula kutoka kwa washiriki na wageni wa tamasha zenyewe. Bw. Geoffrey ambaye ni mchuuzi wa Vibanzi na vyakula vingine, amesema kwamba bashara yake imenawiri ikilinganishwa na siku zingine za kawaida. Pia ameeleza kufurahia kutangamana na wakenya kutoka pembe tofauti za taifa tangu yalipoanza mashindano yenyewe.

Katika sekta ya usafirishaji, wahudumu wa magari ya uchukuzi na bodaboda wamepata faida kubwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri. Wamiliki wa vyumba vya kulala nao wameripoti kuongezeka kwa mahitaji ya malazi katika kipindi hiki cha tamasha. Hoteli, nyumba za wageni, na maeneo mengine ya kukaa yamefurika kutokana na idadi kubwa ya washiriki na wageni wanaohudhuria tamasha hizo.

Kwa ujumla, tamasha za mashindano ya muziki katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara mjini Narok zimeleta faida kubwa kwa wachuuzi na wafanyabiashara mjini Narok. Wafanyabiashara wamefurahi na wanatarajia kuendelea kunufaika wakati tamasha hizi zikiendelea. Makala ya mwaka huu ya tamasha hizi yameandaliwa chini ya kauli mbiu kukuza vipaji kwa ajili ya uvumbuzi na maendeleo ya kitaifa.

 

 

July 17, 2023