BY ISAYA BURUGU 20TH JULY,2023-Usalama umeimarishwa katika sehemu mbali mbali na miji humu nchini huku mandamano yaliyoitishwa na upinzani kupinga gharama ya juu yakimaisha yakiingia siku ya pili hivi leo.Katika jiji la Nairobi,shughuli chache mno zinaonekana kuendelea huku pia kukiwa na magari machache ya uchukuzi wa umma.Maafisa wa polisi wamekita kambi maeneo tofauti ya jiji hilo wakilinda doria.

Baadhi ya maeneo hayo ni yale yaliyotangazwa kuwa wana Azimio la Umoja wangelitumia hivi leo kufanya mikutano na kupanga jinsi ya kufanya mandamano hayo.

Katika mji wa NAKURU hali ni kama hiyo hata ingawa shughuli za kawaida zimeonekana kuendelea japo  kwa kiwango cha chini baadhi ya maduka yakifunguliwa.Wandamanaji wameweka vizuizi katika Barabara kadhaa za kuingia na kutoka jijini humo.

Hali ilivyo katikati mwa jiji la Nairobi siku ya pili ya mandamano tarehe 20 Julai,2023-Picha-Hisani

Katika jiji la Kisumu shughuli chache mno zinaonekana kuendelea huku vijana wakijikusanya kwenye vikundi hata hivyo polisi wanasalia imara katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.

Wakati huo huo makumi ya wenyeji wa kaunti ya Kisumu wamefanya mandamano huku wakikashfu serikali kwa kutoshugulikia gharama ya juu yakimaisha.

Wandamanaji hao waliobeba mabango na matawi wamesema hawana nia ya kuvunja sheria bali nia yao ni kushinikiza haki kutendeka.wandamanaji hao walioimba nyimbo za kumsifu kinara wa Azimio raila Odinga wameandamana kutoka mtaa wa manyatta jijini Kisumu.

July 20, 2023