Rais William Ruto amewaongoza katika uzinduzi wa mpango wa usafiri unaotumia nguvu za umeme, kwenye hafla iliyoandaliwa katika kaunti ya Mombasa. Mpango huo, unaojulikana kama National E-Mobility Programme, una lengo la kuimarisha matumizi ya nguvu za umeme kama njia mbadala ya nishati ya mafuta katika sekta ya usafiri nchini Kenya.
Chini ya Mpango huu, lengo ni kwamba asilimia 5 ya magari yote yaliyosajiliwa nchini Kenya yatakuwa yanatumia nguvu za umeme ifikapo mwaka wa 2030. Hii ni hatua muhimu katika kuelekea kwenye uchumi endelevu na kubadilisha mwelekeo wa nchi kuelekea nishati safi.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamepongeza mpango huo, wakiutaja kama hatua muhimu katika kuboresha hadhi ya Kenya katika ramani ya kimataifa. Waziri wa Biashara na Viwanda nchini Moses Kuria, na mwenzake wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, wametaja uzinduzi huu kama wa kipekee na unaoonyesha kujitolea kwa serikali kuimarisha usafi wa mazingira.
Rais Ruto, katika hotuba yake, amesisitiza umuhimu wa kukumbatia mpango huu kama mojawapo ya njia za kufufua na kurejesha hadhi ya mazingira yetu. Ametaja utumizi wa nguvu za umeme kama njia bora zaidi ya kutatua matatizo ya uchafuzi wa mazingira, hasa yanayotokana na matumizi ya mafuta.
Launch of National E-Mobility Programme, Mombasa County. https://t.co/CGyOJiq1Ln
— William Samoei Ruto, PhD (@WilliamsRuto) September 1, 2023