Kinara wa chama cha Azimio La Umoja, Raila Odinga, ametoa kauli kali kumkosoa Rais William Ruto kuhusu matamshi yake ya hivi karibuni yanayowalenga wanaodaiwa kuhusika na ufisadi nchini Kenya.
Raila Odinga, ambaye alikuwa akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha COTU, Rajab Mwondi, katika kaunti ya Vihiga, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hulka ya viongozi kutoa matamshi yenye utata bila kujali athari zake za kijamii na kisiasa.
Kauli ya Raila Odinga imekuja siku chache baada ya Rais William Ruto kutoa onyo kwa wale anaowaita “wahalifu wa maendeleo” nchini Kenya, akidai kuwa watakabiliwa na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kufungwa jela, kufurushwa nchini, au hata kusafirishwa hadi “Mbinguni.” Matamshi haya ya Rais Ruto yalizua mjadala mkubwa nchini, huku mashirika ya kisheria na yale ya haki za kibinadamu yakijitokeza kumkosoa Rais, kwa kile wanasema ni kuchukua sheria mkononi.
Wakati hayo yakijiri, Odinga aidha amekosoa viongozi wanaodai kuwa yeye na wenzake wanatafuta njia ya kuingia serikalini, akisisitiza kuwa chama cha Azimio La Umoja hakitaki kujiunga na serikali inayodaiwa kuwa iliiba kura ili kuingia mamlakani.