Hali ya Anga

Kongamano la kwanza la hali ya anga barani Afrika limeng’oa nanga asubuhi ya leo, katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa KICC jijini Nairobi. Kongamano hili linapania kuangazia jinsi ya kulikabili tatizo la mabadiliko ya hali ya anga hasa katika bara la Afrika.

Rais William Ruto, ambaye amezindua kongamano hilo, aliwasili katika ukumbi wa KICC akiendesha gari linalotumia nguvu za umeme. Kongamano hili limewaleta pamoja zaidi ya wajumbe 30,000 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, wakiwemo marais zaidi ya 20.

Akizungumza kwenye hotuba yake ya kufungua kongamano hili, Kiongozi wa taifa amesisitiza umuhimu wa bara la Afrika kuchukua hatua madhubuti za kujikwamua kutoka kwa mtego wa utumizi wa nishati zinazochafua mazingira. Ameeleza pia kwamba ushirikiano wa bara la Afrika utawezesha mafanikio katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga, huku akitoa wito kwa mataifa yote kufanya kazi pamoja katika kuleta suluhisho la kudumu kwa changamoto hii.

Kongamano hili linatarajiwa kutoa majadiliano muhimu na mapendekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga barani Afrika.

September 4, 2023