Jopo la kutatua mizozo ya kisiasa nchini (PPDT) limetoa uamuzi wa kusitisha hatua ya chama cha ODM ya kumtimua Mbunge wa Gem, Elisha Odhiambo kutoka kwenye chama hicho. Uamuzi huu unakuja baada ya Mbunge huyo kuwasilisha kesi mbele ya jopo hilo kupinga uamuzi wa ODM.
Mwenyekiti wa jopo hilo, Desmas Nungo, amethibitisha kuwa mbunge huyo amewasilisha kesi mbele yake, ambayo lazima ikamilike kabla ya uamuzi wowote. Msajili wa vyama vya kisiasa nchini vilevile amepewa agizo la kutoidhinisha mabadiliko ya chama cha ODM kuhusu Mbunge huyo.
Chama cha ODM aidha kimepewa agizo la kutomwondoa Mbunge huyo kwenye kamati yoyote ambayo alikuwa mwanachama wake. Elisha alikuwa miongoni mwa wabunge watano wa ODM waliofurushwa kutoka chama hicho wiki iliyopita. Wabunge wengine walioathiriwa na uamuzi huo ni Caroli Omondi (Suba Kusini), Gideon Ochanda (Bondo), Tom Ojienda (Seneta wa Kaunti ya Kisumu), na Phelix Odiwuor Jalang’o (Lang’ata).
Wakati hayo yakijiri, Mbunge wa Kajiado ya Kati, Elijah Kanchory, ametoa shutuma kuhusu uamuzi wa chama cha ODM kuwafukuza wabunge wanaoeleza nia ya kushirikiana na Serikali. Kanchory, ambaye pia ni mbunge wa chama hicho, ameonyesha kutoridhishwa na uamuzi huo na kusema unakwenda kinyume na uhuru wa mahusiano uliowekwa na katiba ya Kenya.
Mbunge huyo ameahidi kushirikiana na viongozi wengine serikalini, ikiwa ni pamoja na rais William Ruto. Hatua yake inaonekana kuhatarisha uanachama wake ndani ya chama cha ODM, lakini Kanchory amesisitiza kuwa ataendelea kufuata kile anachoona ni sahihi.