Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) imemkamata afisa wa polisi wa trafiki katika Kaunti ya Kakamega kwa tuhuma za kuitisha fedha kutoka kwa madereva wa matatu kama “msamaha” baada ya kuyakamata magari yao.

Afisa huyo kwa jina Monyenye Dennis Marunga, ambaye hushika doria barabarni kwa kutumia pikipiki, anadaiwa kuwa na mazoea ya vitendo hivyo vya rushwa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EACC, Marunga amekuwa akikamata magari ya usafiri wa umma na kisha kuitisha fedha kutoka kwa madereva kwa kisingizio cha kuwaachilia huru. Vitendo vyake vya rushwa vimekuwa vikisababisha madereva na wamiliki wa matatu kulazimishwa kutoa pesa kwa afisa huyo ili kuepuka usumbufu na gharama za kisheria.

EACC aidha imeeleza kuwepo kwa lalama nyingi kutoka kwa wahudumu wa uchukuzi wa umma kuhusu hulka ya afisa huyo ya kuwangaisha kwa kutisha fedha za “msamaha” Tume hiyo imeeleza kwamba imejitahidi kufuatilia na kukomesha vitendo vya rushwa na ufisadi nchini, na kukamatwa kwa afisa huyu wa trafiki ni mfano wa juhudi zao za kudhibiti hali hiyo.

 

October 28, 2023