BY ISAYA BURUGU,31ST OCT,2023-Kesi imewasilishwa katika Mahakama Kuu ikitaka kusitisha uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi uliotoa amri ya familia ya Gerishon Kirima kuwafurusha maelfu ya wakazi kutoka eneo la takriban ekari 1,000 katika maeneo ya Njiru, Chokaa na Mihango.
Katika stakabadhi za mahakama, walalamishi hao wanadai kuwa mahakama iliwasilishwa kwa stakabadhi ghushi na familia ya Kirima ilipata hukumu hiyo kwa njia ya udanganyifu.
Mmoja wa walalamishi ambaye ni msimamizi wa shamba la Dominico De Masi, mwanamume aliyeripotiwa kumuuzia marehemu mwanasiasa Gerishon Kirima shamba hilo, amekwenda mahakamani akitaka amri ya kuzuiwa akiteta kuwa hawakuuza shamba hilo kwa marehemu mwanasiasahuyo.katika maombi yake, raia wa Italia Bernado Vicezo De Masi anataka kuhusishwa katika kesi hiyo.
Pia anaiomba mahakama iamuru kuchunguzwa upya kwa hukumu iliyotolewa na Jaji S. Okong’o mnamo Oktoba 23 ambayo ilielekeza wanaomiliki ardhi hiyo LR. Nambari 5908/8 kuondoka kwenye ardhi ifikapo tarehe 31 Desemba, ikishindikana wafurushwe na Wasimamizi wa Kirima Estate.
Msimamizi huyo pia amepinga taarifa kwamba alimuuzia marehemu Kirima shamba hilo miaka ya 1970 na kusema kuwa amekuwa akiwashirikisha maskwota wanaomiliki ardhi yao kwa lengo la kufikia suluhu.