Vikao vya kusikiliza hoja ya kumbandua gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza vimeendelea kwa siku ya pili hivi leo huku baadhi ya wafanyakazi wa kaunti hiyo wakifika mbele ya bunge la seneti kutoa ushahidi wao.

Akitoa ushahidi wake, Afisa mkuu wa Utumishi wa Umma na Utawala katika Kaunti ya Meru Dickson Munene amekanusha madai kwamba Gavana Mwangaza alianzisha na kuwaajiri wakuu wa trafiki.

Hapo baadaye bunge la Seneti linatarajiwa kupiga kura ili kuafiki mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya gavana huyo au kutupilia mbali hoja ya kumtimua.

Wakati huo huo katika bunge hilo la seneti ambapo Maseneta wamependekeza kuanzishwa kwa mchakato wa kumuondoa waziri wa utumishi wa umma nchini Moses Kuria, kufuatia kile walichokitaja kama msururu wa matendo yake ya kuliaibisha taifa.

Maseneta hao walieleza ghadhabu zao katika vikao vya bunge hilo asubuhi ya leo, baada ya waziri Kuria kuchapisha maoni yaliyoonekana kuhitilafiana na shughuli zinazoendelea kwa sasa kwenye bunge hilo, za kusikiliza hoja ya kumbandua gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Hapo jana, waziri Kuria aliweka machapisho kadhaa kwenye mtandao wake wa X, akizungumzia vikao vya kusikiliza hoja ya Kumbandua Gavana Mwangaza, huku akiwataja baadhi ya maseneta na kuwataka kuwa waangalifu ili wasipotoshwe kwenye vikao hivyo.

Hata hivyo seneta wa Nandi Samson Cherargei pia amependekeza kuondolewa kwa waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen.

November 8, 2023