Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) imetangaza kwamba imeanzisha juhudi za kuboresha na kurekebisha miundo mbinu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na KAA siku ya Jumatano, matatizo ya miundo mbinu katika uwanja JKIA yamekuwa yakitatuliwa kwa njia isiyofaa kwa muda mrefu, hali ambayo imesababisha sehemu kadhaa kuwa katika hali mbaya.

KAA imeahidi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa ubora wa miundo mbinu unaangaziwa wakati wa mrekebisho, ili kukidhi viwango vya kimataifa.

Huku hayo yakijiri, Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, ameeleza kumuunga mkono waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, ambaye hivi karibuni alielezea kuwa changamoto za miundo mbinu katika JKIA zinatokana na utepetevu wa serikali iliyopita. Gachagua amesisitiza umuhimu wa kuwajibisha wahandisi wanaoidhinisha miradi isiyoafikia viwango vya ubora na kuwachukulia hatua za kisheria.

Gachagua alikua akizungumza katika kongamano la 30 la Taasisi ya Wahandisi nchini, lililofanyika Hoteli ya Pride In Beach huko Mombasa.

 

November 15, 2023