BY ISAYA BURUGU,20TH NOV,2023-Aliyekuwa Waziri wa Hazina kuu Henry Rotich ameiomba mahakama kumwachilia huru katika kesi ya Ksh.63 bilioni ya Arror na Kimwarer, akisema kwamba simulizi kwamba pesa zilipotea au kuibiwa ni za kubuni.

Anasema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi yake kwa misingi kuwa upande wa mashtaka uliacha kuwaita mashahidi wake wote katika kesi hiyo.Katika mawasilisho yake, Rotich anahoji kuwa amehudumu kwa muda mrefu  kama mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 25 akipanda ngazi hadi kuwa katibu wa kwanza wa baraza la mawaziri la Hazina ya Kitaifa chini ya katiba mpya, “akichochewa na uadilifu, uaminifu na uchapakazi.

Aidha anaeleza kuwa hajawahi kutenda kosa lolote na si mtu ambaye angefanya uhalifu huo mbaya unaodaiwa na upande wa mashtaka.

Kupitia kwa wakili Kioko Kilukumi, Rotich anahoji ni kwa nini Shirika la Kurejesha Mali (ARA) halijawahi kufuatilia pesa zozote zilizopotea au hata kuzizuia.

Rotich anadai zaidi kwamba alikuwa akitenda kulingana na sheria na kufuata ushauri wa mshauri mkuu wa sheria kwa serikali ya Kenya, kwa hivyo hawezi kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu.Uamuzi wa kesi hiyo utatolewa mnamo Desemba 14, 2023.

 

 

November 20, 2023