Jopo la majaji watatu wa Mahakama kuu nchini hii leo walitoa uamuzi kuhusu kesi ya kupinga sheria ya fedha ya mwaka 2023. Majaji hao ambao ni Jaji David Majanja, Jaji Christine Meoli na Lawrence Mugambi, waliwasilisha uamuzi kuhusu vipengee mbalimbali kwenye kesi iliyowasilishwa na walalamishi sita.

Katika uamuzi kuhusu kuhusishwa kwa wakenya katika mchakato wa kuunda sheria hiyo, mahakama ilisema kwamba zoezi la kukusanya maoni ya wakenya lilifuata sheria inavyohitajika kikatiba nchini.

Jaji Christine Meoli alieleza kwamba kamati ya bunge ilihusisha umma na kujumuisha mapendekezo yao kabla ya kuwasilisha mswada wa fedha bungeni. Kuhusiana na ushuru unaotozwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu, mahakama ilisema kwamba ushuru huo hauna msingi wowote kisheria.

Jaji David Majanja alieleza kwamba kuwatenga baadhi ya watu kutoka kwa ulipaji wa ushuru ni ubaguzi na mapendeleo. Mahakama iliagiza kusitishwa kwa utekelezaji wa sheria hiyo ya Nyumba mara moja.

.Mengine yaliyoaangaziwa katika uamuzi wa mahakama ni kwamba spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, hakuvunja sheria yoyote na wala hakuhitaji kupata idhini yoyote kutoka kwa spika wa seneti kabla ya kuruhusu mswada wa fedha kujadiliwa na kuidhinishwa bungeni.

November 28, 2023