BY ISAYA BURUGU 28TH NOV 2023-Rais William Ruto amesema mradi wa nyumba za bei nafuu uliozinduliwa na utawala wake mapema mwaka huu kufikia sasa umebuni nafasi za kazi 120,000.

Rais ambaye alizungumza leo  wakati wa Kongamano la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi (ITUC) lililoandaliwa na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) alipongeza mradi huo wa majaribio kama wa kubadilisha mchezo katika kupambana na ukosefu wa ajira nchini .

Mkuu wa Nchi alitoa hakikisho  kuwa mradi huo wenye utata utaendelea kuunda nafasi nyingi zaidi katika soko la ajira akionyesha kwamba kufikia 2027, mpango huo utakuwa umeunda zaidi ya ajira 500,000.

Alikariri matamshi yake ya hivi majuzi kwamba Kenya ilikuwa katika mazungumzo na Ujerumani ili kubuni nafasi zaidi za ajira katika nchi hiyo ya Ulaya, akiongeza kuwa utawala wake unaharakisha kutumia teknolojia ili kuunda fursa zaidi katika anga ya kidijitali.

Kufuatia uamuzi wa mahakama wa hivi leo uliotangaza kutoza ushuru wa nyumba kuwa kinyume na katiba, Rais Ruto alisema serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa sheria hiyo tata inafuata masharti ya Kikatiba.

November 28, 2023