BY ISAYA BURUGU, 6TH DEC 2023-Serikali imetangaza kuwa watu watano zaidi wameuawa na mafuriko ya El Nino yanayoendelea kote nchini katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 165.Msemaji wa serikali Dkt Isaac Mwaura, akihutubia wanahabari kutoka Kaunti ya Lamu, ameibainisha kuwa kaunti tatu ndizo zilizoathiriwa zaidi kwa sasa, nazo ni; Taita Taveta, Migori, na Meru.
Dkt. Mwaura hata hivyo alibainisha kuwa mvua kubwa inatarajiwa kuendelea kunyesha katika kaunti za Lamu na Tana River pia, kwa hivyo huenda zikaungana na kaunti tatu zilizotajwa katika eneo hatari.
Aliendelea kufichua kuwa mafuriko hayo yamesababisha watu 539,215 kufurushwa kutoka kwa kaya 107,843, hivyo basi serikali imeweka kambi 11 zaidi za kuwahifadhi Tana River (5), Kilifi (4) na Lamu (2).
Msemaji wa Serikali pia alisema kuwa barabara 4, ekari 832 za mashamba, nyumba 23, madaraja 3, shule 3 na afisi ya Chifu huko Lamu zimeharibiwa na mafuriko hayo.