Jaji Mkuu nchini Akutana na Rais Ruto

Jaji Mkuu nchini Martha Koome, na Rais William Ruto wamekutana leo katika ikulu ya Nairobi, katika mkutano ambao unalenga kumaliza mgogoro kati ya serikali ya kitaifa na idara ya mahakama.

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya matamshi ya hadharani kutoka kwa viongozi hao wawili, waliosema wako tayari kushirikiana kutafuta suluhu la kudumu kwa tofauti zilizojitokeza.

Tarehe 15 Januari, Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) chini ya uongozi wa Jaji Mkuu ilitoa taarifa ikiashiria utayari wao wa kuandaa kikao na kiongozi wa taifa. Chini ya saa 24 baadaye, rais Ruto alijibu na kukubaliana na wito huo wa mazungumzo.

Katika siku za hivi karibuni, rais amekuwa akiikosoa mahakama, kwa kuhusika katika njama za kuhujumu utendakazi wa serikali.

Hata hivyo, kikao hicho kimeshutumiwa vikali na kinara wa upinzani Raila Odinga, ambaye ameonyesha wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa idara ya mahakama kutekwa na serikali. Akizungumza baada ya kuzindua mradi wa maji katika shule ya Msingi ya Manda, kaunti ya Lamu, Odinga amesisitiza kuwa kikao cha namna hii hakifai kuandaliwa katika ikulu.

Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetangula, pia ameungana na viongozi hao wawili katika kikao hicho.

 

January 22, 2024