HAITI

Rais William Ruto amekutana na Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry, katika Ikulu ya Nairobi Alhamisi 29.02.2024, kujadili mipango ya ushirikiano kati ya Kenya na Haiti. Kikao hicho kilihudhuriwa na pande zote mbili kwa lengo la kufanikisha mpango wa serikali ya Kenya kuwatuma maafisa 1000 wa polisi kusaidia katika kurejesha amani nchini Haiti.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho, Rais Ruto amesisitiza kuwa Kenya inaendelea kuunga mkono Haiti katika jitihada zake za kukabiliana na magenge ya wahalifu ambayo yamechukua udhibiti wa taifa hilo. Hata hivyo, mkutano huo umefanyika licha ya agizo la mahakama ambalo lilisitisha mpango wa kutuma maafisa wa polisi katika taifa hilo.

SOMA PIA | Serikali yapata pigo jingine baada ya kusitishwa kwa hatua ya kupelekwa kwa maafisa wa polisi 1,000 nchini Haiti.

Uamuzi wa Mahakama uliotolewa na Jaji Chacha Mwita mnamo Januari 26 mwaka huu ulibainisha kwamba Baraza la Kitaifa la Usalama halina mamlaka ya kuamuru kutumwa kwa maafisa wa polisi kwa operesheni hiyo.

February 29, 2024