Maseneta wa Azimio

Maseneta wa mrengo wa walio wachache katika Bunge la Seneti wameeleza wasiwasi wao kuhusu kile walichokitaja kama “utekaji nyara” wa shughuli za bunge hilo na viongozi wakuu wa serikali.

Katika kikao na waandishi wa habari siku ya Jumatatu baada ya kukamilisha kikao cha mashauriano, maseneta hao wakiongozwa na kiongozi wa walio wachache katika seneti, Stewart Madzayo, na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, wametoa kilio chao kuhusu kutengwa kwa upande wao katika shughuli za kuwasilisha miswada inayolenga kusaidia wananchi.

Maseneta hao wamesema kwamba licha ya kumwandikia barua ya malalamiko spika Amson Kingi, hakuna kilichofanyika. Sasa wanamtaka Kingi kujibu barua zote za malalamiko haraka iwezekanavyo ili kushughulikia madai ya upendeleo kwenye sakafu ya nyumba hiyo.

Aidha viongozi hao pia wameeleza ghadhabu yao kuhusu mwenendo wa kuharakisha upitishwaji wa miswada bungeni usiozingatia kwa kina maslahi ya wananchi. Wamekosoa upande wa serikali kwa kuhimiza kupitishwa kwa miswada bila kuhakikisha kwamba inawanufaisha wananchi moja kwa moja.

Wakitoa wito wa kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha usawa katika mchakato wa kuleta mabadiliko kupitia bunge, viongozi hao wa upinzani wameahidi kuendelea kupigania haki za wananchi na kuwasilisha masuala yanayowagusa moja kwa moja.

 

March 4, 2024