Kikao cha Maseneta wote kitaamua hatima ya Naibu Rais Rigathi Gachagua wiki ijayo. Hii ni baada ya hoja ya kutaka kuundwa kwa kamati maalum ya wanachama 11 kuchunguza mashtaka dhidi ya naibu rais kukosa kuungwa mkono.

Kiongozi wa Wengi katika bunge la Seneti Aaron Cheruiyot alikuwa amewataka maseneta kuzingatia kamati teule.

Kufuatia maagizo yaliyotolewa, timu ya wanasheria wa Gachagua imeratibiwa kujibu mashtaka hayo siku ya Jumatatu kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa Jumatano, kwa siku mbili.

Kando na hayo spika wa bunge la seneti Amason Kingi ameahidi  kwamba sheria itafuatwa kikamilifu katika mchakato wa kusikiliza na kuamua kesi ya kubanduliwa kwa naibu wa rais Rigathi Gachagua.

Amesema kuwa ni jukumu la bunge hilo kuhakikisha kuwa uadilifu unadumishwa katika mchakato huo bila kuegemea upande wowote.

Aidha Kingi amewaonya maseneta dhidi ya kuzungumzia suala hilo kwenye mahojiano ya televisheni au mikutano ya hadhara hadi pale litakapojadiliwa na kuamuliwa.

October 9, 2024