Kithure Kindiki

Naibu wa Rais Kithure Kindiki amesisitiza kuwa jukumu lake kuu ni kumsaidia Rais William Ruto katika juhudi za kuliunganisha taifa na kufanikisha malengo ya kitaifa. Akizungumza katika hotuba yake ya mwisho kwenye ofisi ya Wizara ya usalama wa ndani, Kindiki alieleza kuwa Kenya inahitaji uponyaji kutoka kwa migawanyiko iliyoachwa na  mtangulizi wake, Rigathi Gachagua.

Kuhusiana na majukumu yake ya awali kama Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof. Kindiki alisema kuwa sasa ni wajibu wa mrithi wake kushirikiana na asasi za usalama kukabiliana na matukio ya uhalifu, hasa mauaji ya kiholela ya wanawake yaliyoongezeka nchini katika miezi mitatu iliyopita. Kulingana naye, Kenya sasa inaona kupungua kwa visa vya wizi wa mifugo, ugaidi, na uhalifu mwingine.

Naibu wa Rais pia alisifu mafanikio katika kuboresha vifaa vya kisasa vya polisi, mradi ulioanzishwa mwaka wa 2023.Kuhusu suala la pasipoti, Kindiki alieleza kwamba juhudi zake zimesaidia kuondoa mrundiko wa uchakataji na kupunguza muda wa kusubiri kutoka miezi 12 hadi siku saba pekee.

Kindiki pia aliwapongeza maafisa wa serikali kwa kujitolea katika huduma ya umma na kumtaka mrithi wake kushughulikia changamoto za utekaji nyara, kutoweka kwa watu, na mauaji ya wanawake, mambo ambayo yanaendelea kuwa changamoto kwa taifa.

November 8, 2024