Nyuki narok

Serikali ya Kaunti ya Narok imeombwa kuunga mkono juhudi za wakulima wanaofuga nyuki katika kaunti hii ili kuwawezesha kuzalisha asali kwa wingi na kuongeza faida kutokana na kilimo hiki.

Kiongozi wa Shirika la Wakulima wa Nyuki katika Kaunti ya Narok, Bw. Benjamin Lemoi, amesema kuwa sekta ya ufugaji nyuki imetelekezwa katika kaunti hii ikilinganishwa na kaunti nyingine zinazozalisha asali nchini. Bw. Lemoi alieleza kuwa shirika lake, lenye zaidi ya wanachama 6,000, linakabiliwa na changamoto za kuwafikia wakulima kutokana na ukosefu wa miundombinu bora ya usafiri.

Akizungumza katika ofisi za shirika lake la Narok Beekeeping Cooperative Society viungani mwa mji wa Narok, Lemoi pia ametaja tatizo la ukosefu wa vifaa vya kutosha katika kurina asali kama kizingiti kikuu kwenye ukulima huu. Hali hii ameeleza imefanya wakulima wengi kukosa elimu muhimu kuhusu jinsi ya kufaidi na kuboresha kilimo cha nyuki.

Mbali na hilo, Bw. Lemoi ametoa wito kwa wananchi kukumbatia matumizi ya asali na vyakula vingine vya asili kama njia ya kupunguza magonjwa kama saratani na pia katika kupambana na changamoto za kiafya zinazozidi kuongezeka.

November 18, 2024

Leave a Comment