Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nyeri, Mhashamu Anthony Muheria, ameendeleza ukosoaji mkali dhidi ya viongozi wa kisiasa, akitaja matukio ya hivi karibuni ya malumbano ya kisiasa yaliyoshuhudiwa katika hafla za mazishi Magharibi mwa Kenya kama jambo la kusikitisha na lisilofaa.
Muheria aliwakashifu viongozi wa serikali kwa kile alichokiita ukosefu wa heshima ya kimsingi kwa hafla takatifu kama mazishi. Alisema vitendo vya kugeuza hafla za maombolezo kuwa majukwaa ya siasa ni ishara ya mfano mbaya na ni dhihirisho la kukosekana kwa staha na busara miongoni mwa viongozi.
Aidha, Askofu Muheria aliwataka viongozi wa tabaka la kisiasa kutafakari na kujichunguza upya kuhusu adabu zao, akisisitiza kuwa mazishi yanapaswa kuwa wakati wa mshikamano, maombi, na heshima kwa marehemu pamoja na familia yao. Aliongeza kuwa ni jukumu la viongozi kuonyesha mfano bora kwa jamii kwa kuepuka siasa zisizofaa katika mazingira ya maombolezo.
Vilevile, alikosoa matamshi ya baadhi ya viongozi kuhusu utekaji nyara, akisema viongozi wanapaswa kuwa na uvumilivu wanapokosolewa. Alibainisha kuwa tabia ya kutoa semi zenye kushambulia ni dalili ya ukosefu wa ustahimilivu, huku akihimiza umuhimu wa viongozi kuwa na roho ya kukubali mawazo yanayokinzana.