Wakulima wa ngano katika Kaunti ya Narok wanalalamikia ukosefu wa soko la mazao yao licha ya mavuno mengi yaliyotokana na hali nzuri ya hewa mwaka jana.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Stanley Koonyo, wakulima hao wamesema zaidi ya magunia milioni 10 ya ngano yenye uzito wa kilo 90 bado yako maghalani tangu msimu wa kuvuna ulipoanza Agosti 2024. Hadi sasa, hakuna msagaji yeyote aliyeonyesha nia ya kununua mazao hayo.
Koonyo ameilaumu serikali kwa kuwatenga wakulima licha ya wao kuwekeza pakubwa kwenye kilimo cha ngano. Ameeleza kuwa walinunua pembejeo kama mbolea na dawa za kuulia wadudu ili kuhakikisha mavuno bora, lakini juhudi zao zimeambulia patupu kwa kuwa hakuna soko la uhakika.
Alibainisha kuwa ngano inayozalishwa Narok ni asilimia tano pekee ya mahitaji ya nchi, na iwapo uzalishaji ungeongezeka hadi asilimia 10, changamoto za soko zingekuwa kubwa zaidi. Aliitaka idara ya Kilimo kuingilia kati ili kuwasaidia wakulima ambao wengi wao wanakabiliwa na mzigo wa mikopo kutoka kwa taasisi za kifedha.
Kwa upande wake, Mweka Hazina wa Chama cha Wakulima wa Nafaka (CGA) tawi la Narok, Nicholas Mwangi, alieleza kusikitishwa na hali ya mwaka huu, akisema miaka ya nyuma wakulima waliuza mazao yao kwa faida kubwa. Matiko Ole Sadera, mmoja wa wakulima wakubwa wa ngano, alisema maghala yamejaa kabisa na hali hii inawafanya wakose nafasi ya kuhifadhi mazao mapya watakayovuna.
Kaunti ya Narok ni mojawapo ya maeneo yanayoongoza kwa kilimo cha ngano nchini Kenya, hasa katika eneo la Mau ambapo hali ya hewa inafaa kwa kilimo hicho. Wakulima hao sasa wanaitaka serikali kuingilia kati ili kuhakikisha mazao yao yanapata soko na kuwanusuru na hasara inayowakabili.