Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 40, Benard Kipkemoi Kirui, amehukumiwa kifungo cha miaka 150 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watoto wake watatu mnamo mwaka 2019 katika eneo la Lelaitich, Kaunti ya Bomet.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Bomet, Julius Kipkosgei Ng’arng’ar, alitoa hukumu hiyo siku ya Jumatatu, akibainisha kuwa adhabu hiyo inajumuisha vifungo vitatu vya miaka 50, vitakavyotumikwa mfululizo.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Kirui aliwaua wanawe—Amos Kipngetich (12), Vincent Kiprotich (8), na Emanuel Kipronoh (5)—wakati mama yao hakuwa nyumbani. Jaji Ng’arng’ar alitaja mauaji hayo kuwa ya kikatili, akisisitiza kuwa hukumu hiyo inapaswa kuwa onyo kali kwa yeyote anayepanga kutekeleza uhalifu wa aina hiyo.
Hata hivyo, mshukiwa ana siku 14 za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.