Waumini wa Kikatoliki kote ulimwenguni, siku ya leo wanaadhimisha siku ya Jumatano ya Majivu, kuashiria mwanzo wa kipindi cha kwaresma.
Siku ya leo waumini wamepakwa majivu kwenye paji la uso, kama ishara ya toba. Ibada ya misa takatifu ya kuadhimisha siku hii Pia iliandaliwa katika cathedrali ya mt. Yosefu Ngong ambapo askofu wa jimbo katoliki la Ngong Mhashamu John Oballa Owaa, alizindua rasmi kampeni ya kipindi cha kwaresma, ambayo kaulimbiu yake mwaka huu ni Kenya Tunayoitamani.
Katika Homilia yake, askofu Oballa aliwahimiza wakristu kushikilia na kutilia maanani nguzo tatu za msimu huu ambazo ni kutubu, kusali na matendo ya huruma katika jamii.
Aidha baba askofu alisisitiza umuhimu wa kufunga na kuomba huku akiwataka wakristu kutenga kila ijumaa katika msimu huu wa Kwaresma kwa ajili ya kufunga na kuombea taifa la Kenya.