Ngano

Serikali kupitia Bodi ya Uhifadhi wa Nafaka nchini (NCPB) imetangaza kuanza kununua ngano kutoka kwa wakulima wa Kaunti ya Narok kuanzia leo.

Meneja wa NCPB katika Ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa, Bi. Emily Okwai, amesema kuwa mipango yote inayohitajika imekamilika na wakulima watapokea malipo yao kati ya siku 14 hadi 21 baada ya kuwasilisha mazao yao. Bi. Okwai alizungumza mjini Narok baada ya kufanya kikao na wakulima pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Narok, Bi. Joyce Keshe, amesisitiza kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika bei ya ununuzi wa ngano, hivyo wakulima hawapaswi kuwa na wasiwasi. Amesema kuwa gunia la ngano ya gredi ya kwanza litanunuliwa kwa shilingi 5,300, huku gredi ya pili ikiuzwa kwa shilingi 5,200. Aidha, Waziri huyo ameongeza kuwa serikali imepanga kuondoa shahiri lililoko kwenye maghala ili kutoa nafasi zaidi kwa hifadhi zaidi.

SOMA PIA | Wakulima wa ngano wafungua barabara baada ya mazungumzo na Gavana

Wakulima, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Stanley Ole Koonyo, wamepongeza hatua hiyo lakini wameitaka serikali kuhakikisha kuwa malipo yanafanyika kwa haraka. Mwafaka huu unakuja siku chache baada ya wakulima hao kuandamana wakilalamikia ukosefu wa soko la ngano.

March 6, 2025