IEBC

Wakenya 1,356 wameorodheshwa kuwania nafasi za Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na uratibu wa Mipaka (IEBC).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jopo la Uteuzi wa IEBC, Dkt. Nelson Makanda, jumla ya wakenya 37 wamewasilisha maombi ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa tume hiyo, huku wengine 1,319 wakitaka kuwa Makamishna. Kati ya wagombea 37 wa nafasi ya Mwenyekiti, wanawake ni sita na wanaume ni 31, huku watatu kati yao wakiwa ni Watu Wanaoishi na Ulemavu (PWDs).

Jopo la Uteuzi linatarajiwa kuchapisha orodha kamili ya waliotuma maombi na waliokidhi vigezo kabla ya kuanza mchakato wa kuwahoji. Kulingana na Dkt. Makanda, mchakato wa mahojiano kwa wagombea wa nyadhifa za ukamishna utaanza katikati ya mwezi Machi, huku akiahidi kuwa mchakato huo utakuwa wa uwazi ili kuhakikisha watu wenye uadilifu wanateuliwa.

March 6, 2025