Naibu Rais Kithure Kindiki amewahimiza viongozi wa kidini nchini kuikosoa serikali kwa njia ya upendo na heshima, akisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza iko tayari kusikiliza sauti za kila upande, hasa wakati inakosolewa kwa nia ya kujenga.
Akizungumza siku ya Jumanne katika Ukumbi wa KICC wakati wa Mkutano wa Africa Revival Agenda uliohudhuriwa na wachungaji na wahudumu zaidi ya 4,500 kutoka kaunti zote 47, Kindiki alisema serikali na taasisi za kidini zina wajibu wa kushirikiana kwa ajili ya ustawi wa taifa.
“Tumeona mvutano wakati mwingine kati ya serikali na vikundi vya kidini, na sio sawa kwa nchi kwa sababu hakuna mashindano kati ya Mfalme na Nabii. Ofisi hizo mbili ni tofauti lakini zinakamilishana,” alisema Kindiki.
Naibu Rais alieleza kuwa serikali inaliona kanisa kama mshirika mkuu katika juhudi za kuleta mageuzi ya kijamii na kiutamaduni nchini, huku akisisitiza kuwa viongozi wa dini wana jukumu muhimu la kuongoza jamii kiroho na kimadili.
“Msizungumze nasi kana kwamba zaidi ya marekebisho mna masuala mengine. Jukumu lenu liwe ni kuturekebisha na kuturudisha kwa upendo. Sisi ni serikali inayosikiliza, tutarekebisha pale ambapo hatufanyi vizuri,” alisema.
Kindiki pia alisisitiza kwamba serikali inafanya kazi ya kupambana na uhalifu na maovu mengine ya kijamii kwa vitendo, huku kanisa likiendelea kusimama katika maombi na mafundisho ya maadili. Katika hotuba yake, Naibu Rais aliweka bayana kuwa hakuna uhasama baina ya serikali na makanisa, bali ni uhusiano wa kukamilishana katika kutumikia watu wale wale kwa mitazamo tofauti.
“Wafalme wote wenye busara na wacha Mungu hawakuingia vitani kabla ya kuomba ushauri wa manabii. Ndio maana tunahitaji ushirikiano wa kweli kati ya uongozi wa kisiasa na viongozi wa kidini,” aliongeza.
Kauli hii imekuja wakati serikali inaendelea kuandaa bajeti ya mwaka ujao wa kifedha na kushughulikia changamoto mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimaadili.