Umoja wa Mataifa umesema kwamba msaada wa kimataifa wa chakula kwa taifa la Somalia ndiyo sababu pekee iliyopunguza hatari ya njaa katika taifa hilo linalozongwa na machafuko. Hata hivyo shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni la umoja huo WFP, limetahadharisha kwamba ikiwa ulimwengu utasubiri hadi njaa kutangazwa kote ndipo uchukue hatua za dharura, basi muda utakuwa umechelewa na hali itakuwa mbaya.
Naibu mkurugenzi wa WFP nchini Somalia Laura Turner amewaambia waandishi habari akiwa Mogadishu kuwa Somalia haijaondoka katika hali ya hatari, na kwamba wana wasiwasi kuhusu hali mbaya kote katika taifa hilo kwa sasa.
Kulingana na Turner, viwango vya utapiamlo vinasikitisha huku vifo pia vikianza kuongezeka. Afisa huyo wa WFP amesisitiza kuwa msaada wa chakula ndio unaoweza kuzuia njaa, akiongeza kuwa shirika lake linahitaji dola milioni 300 kuwasaidia wananchi kwa kipindi cha miezi sita ijayo.