Mamlaka huru ya utendakazi wa polisi IPOA imesema kuwa itawachukulia hatua za kisheria maafisa waliohusika na mauaji ya watu mbalimbali humu nchini. Kwenye kikao na waandishi wa habari, mwenyekiti wa mamlaka hiyo Ann Makori amedokeza kuwa IPOA inaunga mkono hatua ya rais William Ruto ya kuvunja kitengo maalum cha DCI kinachodaiwa kuhusika na utekaji nyara wa raia wawili wa kigeni. Kuhusiana na mauaji ya mwanahabari wa Pakistan Arshad Sharif anayedaiwa kuwawa na maafisa wa polisi katika kaunti ya Kajiado, Bi. Makori amesema kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichowapelekea maafisa hao kumpiga mwanahabari huyo risasi jana usiku. Kwenye ripoti ya matukio ya polisi inaarifiwa kuwa polisi walikuwa wakitafuta gari lililoibwa Nairobi na kuwa mwanahabri huyo na nduguye walikataa kusimama kwenye kizuizi cha polisi eneo la Magadi. Mauaji ya mwanahabri huyo aliyekuwa na umri wa miaka 50 yameshutumiwa na wanahabari hapa nchini na kimataifa.