Cabinet Secretaries

Mawaziri 22 pamoja na Mkuu wa Sheria wametwaa nyadhifa zao rasmi baada ya kula kiapo cha utumishi katika hafla ya kuapishwa iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi Leo Alhamisi 27.10.2022.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Rais William Ruto mwendo wa Saa tano, ilishuhudia maafisa 24 wakiwemo mawaziri 22, mkuu wa sheria na katibu katika baraza la mawaziri wakila kiapo chao cha kuwatumikia wakenya baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na bunge. Baada ya hafla hii, mawaziri hao sasa wanaanza jukumu lao mara moja katika wizara mbalimbali, kibarua chao cha kwanza ni kuisaidia serikali kupunguza gharama ya Maisha, Pamoja na kusaidia katika kukabiliana na ukame uliotanda kote nchini.

Walioapishwa hii leo ni Pamoja na aliyekuwa kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Bw. Mudavadi ambaye sasa ni mkuu wa mawaziri serikalini, aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi ambaye sasa ndiye mwanasheria mkuu wa Kenya akitwaa wadhifa uliokuwa umeshikiliwa na Paul Kihara.

YouTube player

ORODHA KAMILI

Orodha kamili ya waliokula kiapo kuwatumikia wananchi kama mawaziri ni;

  1. Mkuu wa Mawaziri – Wycliffe Musalia Mudavadi
  2. Waziri wa Usalama na maswala ya ndani – Prof. Kithure Kindiki
  3. Waziri wa Fedha na Mipango – Prof. Njuguna Ndung’u
  4. Waziri wa utumishi wa umma na Jinsia – Aisha Jumwa Katamwa
  5. Waziri wa Ulinzi – Aden Barre Duale
  6. Waziri wa maji, Usafi na Unyunyizaji – Alice Muthoni Wahome
  7. Waziri wa Maswala ya kigeni – Alfred Mutua
  8. Waziri wa biashara na Viwanda – Moses Kuria
  9. Waziri wa Jumuiya ya Afrika mashariki na maendeleo ya maeneo kame – Rebecca Miano
  10. Waziri wa Barabara, uchukuzi na Ujenzi – Onesmus Kipchumba Murkomen
  11. Waziri wa Mazingira na Misitu – Roselinda Soipan Tuya
  12. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji- Zacharia Mwangi Njeru
  13. Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Turathi – Peninah Malonza
  14. Waziri wa Kilimo na maendeleo ya mifugo – Mithika Linturi
  15. Waziri wa Afya – Susan Nakumincha Wafula
  16. Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali – Eliud Owalo
  17. Waziri wa Elimu – Ezekiel Machogu
  18. Waziri wa kawi na Petroli– David Chirchir
  19. Waziri wa maswala ya vijana, Michezo na Sanaa – Ababu Namambwa
  20. Waziri wa vyama vya ushirika na biashara ndogo na zile za kadri – Simon Chelgui
  21. Waziri wa Madini, uchumi wa baharini na uchukuzi wa majini – Salim Mvuria
  22. Waziri wa leba na ulinzi wa kijamii – Florence Bore
  23. Katibu katika baraza la Mawaziri – Mercy Wanjau
  24. Mwanasheria Mkuu – Justin Muturi Njoka

RAIS RUTO |Hakuna sababu ya kutofaulu

Rais William Ruto ameahidi kuwaunga mkono mawaziri wapya katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Akizungumza baada ya kuongoza hafla ya kuapishwa kwa mawaziri hao katika ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema kuwa ni lazima wafanikishe majukumu yao kwani kufeli si chaguo. Ruto pia amewahimiza kuzingatia sheria na katiba ya taifa kikamilifu wanapotekeleza majukumu yao.

October 27, 2022