Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekwenda Marekani, katika ziara ya kwanza ya kiserikali tangu Rais Joe Biden alipoingia madarakani.
Uhusiano baina ya marais hao ulianza kwa kusuasua, hadi kufikia hatua ya Ufaransa kumrudisha nyumbani balozi wake mjini Washington baada ya Marekani kuipiku Ufaransa kwenye zabuni ya kuiuzia Austrialia nyambizi zinazoendeshwa kwa nguvu za nyuklia.
Hata hivyo uhusiano uliboreka baada ya Macron kuibuka kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa Marekani katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Miongoni mwa agenda muhimu kwenye mazungumzo ya Macron na Biden ni mpango wa nyuklia wa Iran, ubabe unaozidi kuongezeka wa China katika ukanda wa Indo-Pasifiki, na kitisho cha ugaidi katika ukanda wa Sahel, lakini suala kubwa zaidi litakuwa vita vya Ukraine na mkakati wa kuisaidia Kiev kuushinda uvamizi wa Urusi.