Huku jumuiya ya Afrika mashariki likiendelea kufanya mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Congo na waasi wa M23, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametoa wito kwa rais wa Rwanda Paul Kagame kusitisha uungaji mkono anayodaiwa kuutowa kwa waasi hao.
Msemaji wa wizara hiyo Ned Price ameeleza kwamba Blinken alizungumza kwa njia ya simu na kiongozi huyo wa Rwanda na kuweka wazi kwamba hatua yoyote ya nje ya kuyaunga mkono makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapaswa kusitishwa.
Aidha Blinken pia amelaani kuzuka tena kwa matamshi ya chuki na kauli za uchochezi zinazotolewa hadharani zikiilenga Rwanda na kukumbusha athari za kutisha za kauli kama hizo, zilizoshuhudiwa mwaka 1994 katika vita vya kimbari vilivyowalenga watu wa jamii ya kabila la Watutsi.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo ameyahimiza mataifa ya Kongo na Rwanda kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi uliopita nchini Angola.