Maelfu ya waumini wa dini ya kikatoliki mjini Vatican wamejitokeza kwa wingi katika Basilica ya Mt. Petro kuanzia asubuhi ya leo, ili kutoa heshima zao za mwisho kwa papa mstaafu Benedict XVI, aliyeaga dunia siku ya Jumamosi.
Mwili wa papa huyo ulikuwa umewekwa katika jeneza lililo wazi, akiwa amevikwa mavazi mekundu ya maombolezo ya upapa na kilemba chenye ncha za dhahabu kichwani. Papa mstaafu Benedict, anatarajiwa kuzikwa siku ya alhamisi wiki hii, ila mwili wake utasalia katika basilica hiyo ya Mt. Petro kwa siku tatu ili kuwapa waumini nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.
Kiongozi huyo wa kidini mwenye usuli wa kijerumani, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 95, alihudumu kama papa na kiongozi wa kanisa katoliki kwa kipindi cha miaka nane kabla ya kustaafu mwaka wa 2013.
Mrithi wake Papa Francis ataongoza mazishi siku ya Alhamisi katika uwanja wa St. Peters Square, kabla ya mwili wake kuzikwa katika makaburi yaliyoko chini ya Basilica ya Mt. Petro.