Idadi kubwa ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeutolea wito utawala wa Taliban nchini Afghanistan kuondoa mara moja vikwazo vyote Vinavyowakandamiza wasichana na wanawake ikiwa ni pamoja na marufuku ya wanawake kutofanya kazi katika mashirika ya misaada.
Taarifa ya pamoja kutoka kwa wajumbe 11 kati ya 15 wa baraza hilo imesema wafanyakazi wa kike ni muhimu katika kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu kwa sababu wanatoa huduma muhimu za msaada kwa wanawake na wasichana ambao wanaume hawawezi kuwafikia.
Rais wa sasa wa Baraza la Usalama, Balozi wa Japan Kimihiro Ishikane, alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari akiwa pamoja na wanadiplomasia kutoka Albania, Brazil, Ecuador, Ufaransa, Gabon, Malta, Uswisi, Uingereza, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wanachama wanne wa Baraza la usalama ambao hawakuunga mkono wito huo ni pamoja na Urusi, China, Ghana na Msumbiji.