Aliyekuwa waziri wa elimu nchini Profesa George Magoha ameaga dunia. Magoha ameaga dunia jioni ya leo Jumanne 24. Januari 2023 katika hospitali ya Nairobi akiwa na umri wa miaka 71 baada ya kuugua kwa ghafla.
Prof. Magoha aliongoza wizara ya elimu kwa kipindi cha miaka 5 katika serikali iliyopita kuanzia Machi 26, 2019 na kuhudumu hadi Oktoba 27, 2022 kabla ya kuelekea katika chuo kikuu cha Maseno ambapo alikua akihudumu kama mhadhiri katika kitivo cha masomo ya utabibu.
Kulingana na rafiki wa Karibu wa Prof Magoha, Prof. Walter Mwanda aliyetoa taarifa kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya kudhibitishwa kwa kifo chake, amesema kuwa profesa Magoha alifariki dakika chake baada ya kuwasili katika chumba cha wagonjwa Mahututi katika Hospitali ya Nairobi, alikokimbizwa baada ya kupata tatizo la shinikizo la damu. Prof Walter ameeleza kuwa Magoa alikuwa amewaita jamaa zake wa karibu kupitia kwa mkewe mapema leo, kabla ya kuzidiwa na tatizo hilo lililomfanya kuzirai mara nne kabla ya kufariki.
Historia fupi kumhusu mwendazake Aliyekuwa waziri wa Elimu nchini Prof George Albert Omore Magoha ni kwamba alizaliwa tarehe mosi mwezi Januari mwaka 1952. Baada ya kumaliza Masomo yake, Magoha alihudumu katika nyadhifa mbalimbali kuanzia katika vyuo vikuu, akihudumu kama naibu Chansela wa chuo kikuu cha Nairobi kwa kipindi cha Miaka kumi, baadaye akaelekea katika baraza la kitaifa la Mitihani KNEC, alikokua akihudumu kabla ya uteuzi wake katika wizara ya elimu mwaka wa 2019.