Abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Narok na Mai Mahiu walilazimika kukesha barabarani usiku wa kuamkia leo, baada ya wafugaji kufunga barabara hiyo eneo la Suswa. Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa tatu usiku baada ya kondoo wa mfugaji mmoja kugongwa na gari na kuuwawa.
Wafugaji hao, wakiwa na ghadhabu, walikusanyika katika eneo la tukio na kufunga barabara kwa kuwasha moto na kushinikiza kufidiwa kwa hasara waliyoipata. Licha ya juhudi za maafisa wa polisi na viongozi wa eneo kujaribu kuzungumza nao, mazungumzo hayo hayakufanikiwa.
Madai ya wafugaji yalikuwa kwamba dereva aliyehusika na ajali hiyo alipaswa kuwajibika kabla ya kufungua barabara. Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari pande zote za barabara, huku abiria wakisalia mateka wa hali hiyo kwa zaidi ya saa sita.
Hatimaye, mwendo wa saa tisa asubuhi, maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya wafugaji hao na kufanikisha kufunguliwa kwa barabara.