Afisa wa Mauaji kushtakiwa

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini (DPP) ameidhinisha mashtaka dhidi ya afisa wa polisi anayedaiwa kuwaua watu wawili katika mzozo wa baa mjini Nakuru mwezi Disemba Mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na DPP, afisa huyo kwa jina Nichola Musau atashtakiwa kwa makosa mawili ya mauaji baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kubaini kuwa kuna ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Musau, alikamatwa tarehe 12 mwezi Jana na kuwasilishwa mahakamani, hata ingawa kwa wakati huo hakusomewa shtaka la mauaji. Inelezwa kwamba afisa huyo alihusika katika mauaji ya mmiliki wa klabu ya burudani ya NaxVegas, Laura Kwisira, na mhudumu wa baa, Ann Maina, kufuatia mzozo wa bili ya Shilingi 16,000. Afisa huyo pia anadaiwa kuwapiga risasi walinzi wawili wa klabu hiyo, ambapo mmoja wao bado amelazwa hospitalini akipokea matibabu.

Nyaraka za Mahakama zinaeleza kwamba DPP ametoa idhibati ya mashtaka ya mauaji kusomwa dhidi ya polisi huyo ambaye amekuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Nakuru Central. Mshukiwa huyo alifikishwa kortini kwa mara ya tatu siku ya Jumanne 9.01.2024. Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wycliffe Omwenga uliomba aendelee kuzuiliwa kwa siku 14 katika Kituo cha Polisi cha Naivasha.

 

January 10, 2024