Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu amehukumiwa kifungo cha miaka 12 gerezani au kulipa faini ya Ksh. milioni 52.5.

Gavana huyo wa zamani alipatikana na hatia ya mgongano wa maslahi katika kesi ya ufisadi ya Ksh.588 milioni. Katika hukumu hiyo katika Mahakama ya Milimani hii leo, Waititu vile vile alizuiliwa kuwania kiti chochote cha kisiasa kwa muda wa miaka 7.

Waititu alishtakiwa pamoja na mkewe, Susan Ndung’u, ambaye alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya Ksh.500,000.Mahakama pia iliwatia hatiani kwa mashtaka yanayohusiana na ufisadi lakini ikawaachilia kwa makosa matatu ya ulanguzi wa fedha.

Mshtakiwa mwenzao,ambaye ni mkurugenzi wa Testimony Enterprises Limited Charles Chege, pia ameadhibiwa kwa kifungo cha miaka 9 au kulipa faini ya Ksh.295 milioni.

Beth Wangeci, mkurugenzi wa pili katika Testimony Enterprises Limited pia amepigwa faini ya Ksh.1 milioni au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

February 13, 2025